Wabunge
wapenzi wa Simba wanatarajia kuumana wikiendi hii, ikiwa ni mechi
mahsusi kwa ajili ya kuchangisha fedha za kusaidia wahanga wa tetemeko
la ardhi lililotokea hivi karibuni huko mkoani Kagera.
Mbali
na mechi hiyo pia kutakuwa na mechi za ufunguzi baina ya Bongo Muvi
dhidi ya Bongo Fleva, pia kutakuwa na mechi ya netiboli
itakayoikutanisha timu ya bunge dhidi ya ile ya Shirika la Utangazaji
Tanzania (TBC), mechi zote hizo zitapigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.
Mbunge
wa Sengerema na Mwenyekiti wa Bunge SC, William Ngeleja ameweka wazi
kuwa licha ya wabunge hao kuchangia kiasi cha Sh milioni 85 kupitia
posho zao wakiwa bungeni lakini bado wameona kuna msaada zaidi
unahitajika kwa ajili ya angalau kurejesha hali ya maisha ya awali ya
Kagera ndiyo maana kumeandaliwa mechi hizo.
“Lengo
letu ni kukusanya fedha za kuwasaidia ndugu zetu wa kule Kagera,
angalau warejewe na hali waliyokuwa nayo awali, tangu awali kule bungeni
kupitia posho zetu tulishachanga milioni 85 lakini tunahitaji kuongeza
zaidi misaada kwao ndiyo maana tumeandaa mechi hii ili kila Mtanzania
kupitia kiingilio alichonacho naye ashiriki kuwakomboa ndugu zetu hawa.
“Vikosi
vitakuwa vikali kwa ajili ya kutoa burudani ya kutosha, huku kwetu
Simba tutakuwa na Kassim Majaliwa, Hamis Kigwangwala, Kaizer Makame na
wengine. Kule Yanga nao watakuwa na Ridhiwani Kikwete, Anthony Mavunde,
Mwigulu Nchemba na wengine wengi.
“Bongo
Muvi wao watakuwa na kina Ray Kigosi, JB, Muhogo Mchungu, Dk. Cheni na
wengine, lakini Bongo Fleva wao watakuwa na kina Tundaman, Ali Kiba,
Diamond, KR Mullah na wengine. Kuhusu mgeni rasmi, tunakamilisha
taratibu na muda si mrefu tutamtangaza,” alisema Ngeleja ambaye ni
Mbunge wa Jimbo la Sengerema.
Tayari
viingilio vya mechi hiyo itakayopigwa Jumapili hii vimeshawekwa wazi
ambapo Sh 3,000 itakuwa kwa viti vya rangi ya bluu na kijani, Sh 10,000
na 15,000 itakuwa kwa ajili ya viti vya rangi ya machungwa huku Sh
50,000, 100,000 na 200,000 ikiwa ni kwa V.I.P C, B na A.
Lakini
kwa viti 50 pekee maalum vitakavyokuwa karibu na mgeni rasmi wa mechi
hiyo ambaye atatajwa baadaye, kila kimoja kitalilipiwa Sh 1,000,000.
Chanzo saleh jembe.
Comments
Post a Comment